Tuesday, October 9, 2012

RISALA YA SHULE KWA MGENI RASMI KATIKA MAHAFALI YA TATU (3) YA KIDATO CHA NNE (4) MWAKA 2012.



Mheshimiwa Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya shule, Wazazi, Walimu, Wanafunzi, Mabibi na Mabwana.Kwa niaba ya shule ya sekondari ya Tushikamane, ninayo furaha kubwa kukukaribisha wewe pamoja na wageni uliongozana nao, ili uweze kuona na kusikia mambo yanayotendeka hapa shuleni, hususani shughuli za kitaaluma na ujenzi kwa ujumla. Tunasema karibuni sana.

Mheshimiwa mgeni rasmi, shule yetu ilianzishwa mwaka 2007 katika majengo ya Kanisa Katoliki yaliyopo Kata ya Kilakala, tunaushukuru uongozi wa Kanisa kwa kuthamini Elimu. Shule hii ilianzishwa chini ya Mkuu wa Shule, Mwalimu Flora Masoy ambaye aliweka misingi mizuri ya kitaaluma na kinidhamu, tunatoa pongezi za dhati kwake na familia yake kwa ujumla.

Mheshimiwa mgeni rasmi, shule hii ilianza na wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60, ikiwa na walimu 9; wanawake 6, na wanaume 3. Kwasasa shule hii ina wafanyakazi wa ajiriwa 30 na wasio wa ajiriwa 6; wafanyakazi wa ajiriwa walimu ni 29, mfanyakazi 1 sio mwalimu. Wafanyakazi wasio wa ajiriwa wanne (4) ni walimu na wawili (2) sio walimu; wafanyakazi hawa wanalipwa posho  kutoka katika mifuko ya shule.

Mheshimiwa mgeni rasmi, shule yetu ina michepuo ya sayansi na sanaa,ina mradi wa ujenzi wa vyumba viwili (2) vya madarasa na nyumba moja (1) ya mwalimu ambao unaendeshwa kwa nguvu za wananchi na serikali. Katika kipindi cha miaka mitano (5) tumeweza kujenga vyumba vya madarasa kumi na nne (14) na jengo la choo cha wanafunzi lenye matundu kumi (10). Vilevile tuna na mradi wa kisima cha maji ambao unaendeshwa kwa michango ya wazazi, kwasasa mradi huu umesimama kwa kukosa pesa kwa vile wazazi wengine bado hawajachangia; zinahitajika Shilingi za Kitanzania laki sita (Tsh.600, 000) kukamilisha sehemu ya mradi ilio bakia.

Mheshimiwa mgeni rasmi, shule imefanikiwa kupeleka wanafunzi kidato cha tano (5) na vyuo mbali mbali ; mwaka 2010 wanafunzi  watatu (3) na mwaka 2011 wanafunzi saba (7) walijiunga na kidato cha tano (5). Mwaka huu tunategemea kupeleka wanafunzi wengi zaidi kidato cha tano (5). Jumla ya wanafunzi waliojiunga vyuo mbalimbali kwa mwaka 2010 na mwaka 2011 ni kumi na tano (15).

Mheshimiwa mgeni rasmi, katika michezo, shule imeweza kutoa wanafunzi kuunda timu ya mpira wa miguu ya ‘copa coke-cola’ ya mkoa wa Morogoro, kushirki mashindano ya UMISETA ngazi ya Mkoa na pia tumeweza kushiriki mashindano ya kitamaduni yanayo endeshwa na Fransalian, na kushika nafasi ya pili kwa vipindi viwili tofauti. Shule imeweza pia kuboresha nidhamu ya wanafunzi.
Mheshimiwa mgeni rasmi, pamoja na mafanikio haya, shule yetu ina matatizo mbalimbali.

Mheshimiwa mgeni rasmi, tuna tatizo la upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; kwani kwasasa kitabu kimoja (1) kinatumiwa na wanafunzi ishirini na tatu (23), hii imepelekea wanafunzi kushindwa kujisomea, kwani kila mwanafunzi anatakiwa kuwa na kitabu kimoja (1) katika somo husika.

Mheshimiwa mgeni rasmi, pia tuna tatizo la upungufu wa vifaa vya maabara,kama vile; meza za kufanyia ‘practical’ na kabati za kuhifadhia vifaa mbalimbali vya maabara, hii inapelekea wanafunzi kuwa na mazingira magumu ya kujifunza kwa vitendo.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tatizo jingine ni upugufu wa walimu hasa wa masomo ya sayansi, kwani kwasasa shule ina walimu wasayansi wanne (4) tu, ukilinganisha mahitaji ya shule ya walimu kumi na tatu (13) wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa mgeni rasmi, vilevile tuna tatizo la ukosefu wa jengo la utawala na maabara, hii imepelekea shule kutumia baadhi ya vyumba vya madarasa kama ofisi ya walimu na maabara.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tatizo jingine ni maji, shule haina kisima cha maji, hivyo kupelekea shule kuingia gharama kubwa ya kuagiza maji kwaajili ya usafi na umwagiliaji wa miti.

Mheshimiwa mgeni rasmi, tuna tatizo pia la uzio, shule yetu haina uzio ambao ungeweza kutusaidia kudhibiti usalama wa mali za shule na nidhamu kwa wanafunzi, hii imepelekea shule kuibiwa samani zake mbalimbali.
Mheshimiwa mgeni rasmi, kupitia kwako tunaomba utusaidie kupata jengo la utawala na maabara, vifaa vya maabara, kisima cha maji na vitabu vya kiada na ziada.

Mheshimiwa mgeni rasmi, tunapenda kuishukuru serikali kupitia Halimahauri ya Manispaa ya Morogoro, Ofisi ya Kata ya Sabasaba kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa shule, vilevile tunapenda kuishukuru tena serikali kupitia kwa Maafisa elimu wetu wa Mkoa na Manispaa kwa kutuletea walimu, wakiwemo walimu wachache wa masomo ya sayansi.

             Mheshimiwa mgeni rasmi, tunatumaini kuwa utatusaidia kutatua matatizo katika shule yetu             ili tuweze kuboresha zaidi kiwango cha elimu. Aksante sana kwa kufika katika Mahafali haya,             kwani tunatambua kuwa una majukumu mengi ambayo umeyaacha. Tuna shukuru sana,                     Karibu tena Shule ya Sekondari ya Tushikamane.


          Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Tushikamane Sekondari
                             Aksanteni sana kwa kunisikiliza.


No comments:

Post a Comment