Ndugu Mgeni rasmi, Walimu,
Wanafunzi wenzetu, Wazazi, Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha nne, tunayo
heshima na furaha kubwa , kukukaribisha ili ushiriki nasi katika siku hii
muhimu na kusikia mafanikio mbalimbali kwa kipindi chote cha masomo yetu hapa
shuleni.
Shukrani zetu za pekee na za dhati ziende kwa uongozi
mzima wa Shule na walimu wetu wote kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa kutufundisha, hivyo tumefundishika vyema;
kwasababu tupo tofauti sana na tulivyokuja hapa mwezi januari 2009.
Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa
wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60. Mpaka leo tunapohitimu tupo
wanafunzi 90; kati yao wavulana ni 43, na wasichana 47. Wengine wameshindwa
kuhitimu nasi siku ya leo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro,
ujauzito na kuhama shule. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema wa
Baraka kwa ulinzi wake kwetu hadi leo hii tunahitimu kidato cha nne.
Ndugu mgeni rasmi,
elimu hii ya kidato cha nne imetupatia
msingi mzuri wa kujiunga na Elimu ya juu, pia imetujengea uwezo mzuri wa
kujitambua na kufikiri, kufanya kazi vizuri na kufanya maamuzi sahihi; pia imetuwezesha
sisi wanafunzi kupata elimu ya mambo mbalimbali
kupitia masomo tunayo fundishwa hapa shuleni, mfano; tumepata elimu ya
uraia, historia ya mambo mbalimbali katika nchi yetu na dunia kwa ujumla, pia
tumeweza kupata uelewa kuhusu afya na magonjwa,
usalama katika mazingira yetu, Kilimo, Maumbile ya nchi, hali ya hewa, misitu,
na viwanda. Vilevile tumeelewa umuhimu
wa kusoma vitabu mbalimbali kwa lengo la kupata ujuzi wa kuinua uchumi wetu wa
taifa.
Ndugu mgeni rasmi, mafanikio hayo yamepatikana
kwasababu ya ushirikiano mzuri kati yetu na walimu wetu. Tangu tujiunge na shule
hii tukiwa kidato cha kwanza tumefanya majaribio na mitihani ya mara kwa mara
jambo lililo tusaidia kuinua taaluma yetu.Tunawashukuru sana walimu wetu, tuna waahidi kufanya vizuri
katika mitihani yetu ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu, na Mungu awabariki
sana.
Ndugu mgeni rasmi, tumepata changamoto mbalimbali
wakati wa maisha yetu ya kielimu hapa shuleni, kama ifuatavyo;
Ndugu mgeni rasmi, tuna changamoto ya upungufu wa
vitabu vya kiada na ziada; hii imepelekea kushindwa kujisomea vizuri, kwani
kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya ishirini (20).
Ndugu mgeni rasmi, changamoto nyingine ni upungufu wa
vifaa vya maabara, hii inapelekea kuchangia kifaa kimoja, hivyo tuna tumia muda
mwingi sana kujifunza na kumuelewa mwalimu.
Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa
walimu, hasa wa masomo ya sayansi; hii imepelekea kutomaliza ‘syllabus’ kwa wakati.
Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa samani
za shule, kama vile; madawati kwa ajili ya wanafunzi, viti na meza kwa ajili ya
walimu; hii imepelekea baadhi ya wanafunzi wenzetu kukaa wawili kwenye dawati
moja.
Ndugu mgeni rasmi, maji ni changamoto hapa shuleni, kwani shule
haina kisima cha maji, hii imepelekea shule kununua maji kwa gharama kubwa,
ambayo hayatoshelezi mahitaji ya shule, kama vile usafi; hususani kwa upande wa
vyoo, bila kuwa na maji ya kutosha tutapata magonjwa ya mlipuko, kama vile
kipindupindu.
Ndugu mgeni rasmi, changamoto ya vifaa
vya michezo; kama unavyojua kuwa michezo ni afya, shule yetu ina upungufu mkubwa
wa vifaa vya michezo kama vile; mipira ya miguu, pete na mikono, pia hatuna
milingoti ya chuma kwaajili ya magoli ya viwanja vya michezo yote tunayocheza
hapa shuleni.
Ndugu mgeni rasmi, tunashukuru uongozi
wa shule hii, walimu na wazazi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia
maendeleo ya shule yetu; kwa upande wa masomo ya sayansi; shule imeweza kutenga
chumba kimoja cha darasa kitumike kama maabara japo kuwa kuna upungufu mkubwa
wa vifaa.
Ndugu mgeni rasmi, tunayo matumaini kwamba maombi yetu
umeyasikiliza na utayaatekeleza, maana tunajua kwamba wewe unaweza kupitia
Hlimashauri unayo isimamia, asante sana.
Mwisho tunaomba msamaha wa dhati toka moyoni mwetu kwa
Walimu, Wanafunzi wenzetu na Wazazi pale tulipoenda kinyume na matazamio yenu,
kwani watu wakiishi pamoja tofauti lazima ziwepo, tunatumaini mtapokea msamaha
wetu, nasi hatuna jambo lolote baya kwenu.
Ndugu mgeni rasmi, tuna kushukuru sana kwa kufika
katika Mahafali yetu, kwani tunatambua kuwa unamajukumu mengi ambayo umeyaacha
na kuwepo hapa kwaajili yetu.
Karibu tena Tushikamane, na Mungu
akubariki sana.
Mungu
ibariki Tanzania, Mungu ibariki Tushikamane Sekondari
Nashukuruni kwa
kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment