Mheshimiwa Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa
Bodi ya shule, Wazazi, Walimu, Wanafunzi, Mabibi na Mabwana.Kwa niaba ya shule
ya sekondari ya Tushikamane, ninayo furaha kubwa kukukaribisha wewe pamoja na
wageni uliongozana nao, ili uweze kuona na kusikia mambo yanayotendeka hapa
shuleni, hususani shughuli za kitaaluma na ujenzi kwa ujumla. Tunasema karibuni
sana.
Mheshimiwa mgeni rasmi, shule yetu
ilianzishwa mwaka 2007 katika majengo ya Kanisa Katoliki yaliyopo Kata ya
Kilakala, tunaushukuru uongozi wa Kanisa kwa kuthamini Elimu. Shule hii
ilianzishwa chini ya Mkuu wa Shule, Mwalimu Flora Masoy ambaye aliweka misingi
mizuri ya kitaaluma na kinidhamu, tunatoa pongezi za dhati kwake na familia
yake kwa ujumla.
Mheshimiwa mgeni rasmi, shule hii
ilianza na wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60, ikiwa na walimu 9;
wanawake 6, na wanaume 3. Kwasasa shule hii ina wafanyakazi wa ajiriwa 30 na
wasio wa ajiriwa 6; wafanyakazi wa ajiriwa walimu ni 29, mfanyakazi 1 sio
mwalimu. Wafanyakazi wasio wa ajiriwa wanne (4) ni walimu na wawili (2) sio
walimu; wafanyakazi hawa wanalipwa posho kutoka katika mifuko ya shule.
Mheshimiwa mgeni rasmi, shule yetu ina
michepuo ya sayansi na sanaa,ina mradi wa ujenzi wa vyumba viwili (2) vya
madarasa na nyumba moja (1) ya mwalimu ambao unaendeshwa kwa nguvu za wananchi
na serikali. Katika kipindi cha miaka mitano (5) tumeweza kujenga vyumba vya
madarasa kumi na nne (14) na jengo la choo cha wanafunzi lenye matundu kumi
(10). Vilevile tuna na mradi wa kisima cha maji ambao unaendeshwa kwa michango
ya wazazi, kwasasa mradi huu umesimama kwa kukosa pesa kwa vile wazazi wengine
bado hawajachangia; zinahitajika Shilingi za Kitanzania laki sita (Tsh.600, 000)
kukamilisha sehemu ya mradi ilio bakia.
Mheshimiwa mgeni rasmi, shule
imefanikiwa kupeleka wanafunzi kidato cha tano (5) na vyuo mbali mbali ; mwaka
2010 wanafunzi watatu (3) na mwaka 2011
wanafunzi saba (7) walijiunga na kidato cha tano (5). Mwaka huu tunategemea
kupeleka wanafunzi wengi zaidi kidato cha tano (5). Jumla ya wanafunzi
waliojiunga vyuo mbalimbali kwa mwaka 2010 na mwaka 2011 ni kumi na tano (15).
Mheshimiwa mgeni rasmi, katika
michezo, shule imeweza kutoa wanafunzi kuunda timu ya mpira wa miguu ya ‘copa
coke-cola’ ya mkoa wa Morogoro, kushirki mashindano ya UMISETA ngazi ya Mkoa na
pia tumeweza kushiriki mashindano ya kitamaduni yanayo endeshwa na Fransalian,
na kushika nafasi ya pili kwa vipindi viwili tofauti. Shule imeweza pia
kuboresha nidhamu ya wanafunzi.
Mheshimiwa mgeni rasmi, pamoja na
mafanikio haya, shule yetu ina matatizo mbalimbali.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tuna tatizo
la upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; kwani kwasasa kitabu kimoja (1) kinatumiwa
na wanafunzi ishirini na tatu (23), hii imepelekea wanafunzi kushindwa
kujisomea, kwani kila mwanafunzi anatakiwa kuwa na kitabu kimoja (1) katika
somo husika.
Mheshimiwa mgeni rasmi, pia tuna
tatizo la upungufu wa vifaa vya maabara,kama vile; meza za kufanyia ‘practical’
na kabati za kuhifadhia vifaa mbalimbali vya maabara, hii inapelekea wanafunzi
kuwa na mazingira magumu ya kujifunza kwa vitendo.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tatizo jingine
ni upugufu wa walimu hasa wa masomo ya sayansi, kwani kwasasa shule ina walimu wasayansi
wanne (4) tu, ukilinganisha mahitaji ya shule ya walimu kumi na tatu (13) wa
masomo ya sayansi.
Mheshimiwa mgeni rasmi, vilevile tuna
tatizo la ukosefu wa jengo la utawala na maabara, hii imepelekea shule kutumia baadhi
ya vyumba vya madarasa kama ofisi ya walimu na maabara.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tatizo jingine
ni maji, shule haina kisima cha maji, hivyo kupelekea shule kuingia gharama kubwa
ya kuagiza maji kwaajili ya usafi na umwagiliaji wa miti.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tuna tatizo
pia la uzio, shule yetu haina uzio ambao ungeweza kutusaidia kudhibiti usalama
wa mali za shule na nidhamu kwa wanafunzi, hii imepelekea shule kuibiwa samani
zake mbalimbali.
Mheshimiwa mgeni rasmi, kupitia kwako
tunaomba utusaidie kupata jengo la utawala na maabara, vifaa vya maabara,
kisima cha maji na vitabu vya kiada na ziada.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tunapenda kuishukuru
serikali kupitia Halimahauri ya Manispaa ya Morogoro, Ofisi ya Kata ya Sabasaba
kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa shule, vilevile tunapenda kuishukuru tena
serikali kupitia kwa Maafisa elimu wetu wa Mkoa na Manispaa kwa kutuletea walimu,
wakiwemo walimu wachache wa masomo ya sayansi.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki
Tushikamane Sekondari
Aksanteni sana kwa
kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment